Tafakuri ya Pili, Āyat 9:40: Ushindi unatoka kwa Mwenyezi Mungu

اِلاَّ تَنصُرُوهُ فَقَدْ نَصَرَهُ اللَّهُ إِذْ أَخْرَجَهُ الَّذِينَ كَفَرُوا ثَانِيَ اثْنَيْنِ إِذْ هُمَا فِي الْغَارِ إِذْ يَقُولُ لِصَاحِبِهِ لاَ تَحْزَنْ إِنَّ اللَّهَ مَعَنَا فَأَنزَلَ اللَّهُ سَكِينَتَهُ عَلَيْهِ وَأَيَّدَهُ بِجُنُودٍ لَمْ تَرَوْهَا وَجَعَلَ كَلِمَةَ الَّذِينَ كَفَرُوا السُّفْلَى وَكَلِمَةُ اللَّهِ هِيَ الْعُلْيَا وَاللَّهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ
(التوبة/40)

Kama hamtamsaidia, basi Mwenyezi Mungu alimsaidia walipomtoa wale waliokufuru. Alipokuwa wa pili katika wawili, alipomwambia sahibu yake: Usihuzunike, hakika Mwenyezi Mungu yuko pamoja nasi. Mwenyezi Mungu akamteremshia utulivu Wake, na akamsaidia kwa majeshi msiyoyaona. Na akilifanya neno la wale waliokufuru kuwa chini, na neno la Mwenyezi Mungu ndilo la juu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
(Sūratut Tawba; 9:40)

 

Aya hii ilishuka katika kuwaonya Waislamu ambao walikuwa wanakaidi kupigana katika vita vya Tabuk. Mwenyezi Mungu anawakumbusha kwamba kama hawatamsaidia Mtukufu Mtume (s) na kazi yake, wala haitarudi nyuma. Mwenyezi Mungu ataisaidia kama vile tu ambavyo amewahi kufanya katika nyakati za nyuma. Rejea hii katika aya hii ni kuhusu msaada wa Mwenyezi Mungu wakati Mtukufu Mtume (s) alipokuwa kwenye pango la Thaur wakati akiwa anahama kutoka Makkah kwenda Madina. Qur’ani pia inarejea kwenye tukio hili katika Suratul-Anfal, Sura ya 8 aya ya 30.

Maadui wa Makkah walikuwa wamepanga kumuuwa Mtukufu Mtume (s) ili kuzuia kuenea kwa Uislamu. Mwenyezi Mungu akamjulisha Mtukufu Mtume (s) juu ya njama yao na akaondoka Makkah wakati wa usiku ambapo Imam Ali (a) akalala kwenye kitanda chake Mtume. Mtukufu Mtume (s) aliandamana na Abu Bakr katika safari hii. Walitafuta hifadhi kwenye pango la Thaur na wakakaa humo kwa muda wa siku tatu ili maadui wasiweze kuwafuatilia. Wakati wakiwa ndani ya pango hilo, Abu Bakr alikuwa na wasiwasi kuhusu kugunduliwa kwao na Mtukufu Mtume (s) akamhakikishia usalama kwa kumwambia : “Usihuzunike, Mwenyezi Mungu yupo pamoja nasi.” Kuthibitishiwa huku kulileta zawadi ya utulivu kutoka kwa Mwenyezi Mungu na msaada wa majeshi yasiyoonekana. Ule muujiza wa kiota cha njiwa na utando wa buibui pale mlangoni mwa pango ni ushahidi wa jinsi majeshi ya Mwenyezi Mungu yalivyofanya kazi ya kumlinda Mtukufu Mtume (s) na kazi yake.

Aya hii inawakumbusha Waislamu kwamba dini ya Mwenyezi Mungu – Neno Lake – siku zote itakuwa yenye ushindi, licha ya juhudi zote za maadui katika kuipinga. Kama Mwenyezi Mungu anavyosema katika aya nyingine:

يُرِيدُونَ لِيُطْفِئُوا نُورَ اللَّهِ بِأَفْوَاهِهِمْ وَاللَّهُ مُتِمُّ نُورِهِ وَلَوْ كَرِهَ الْكَافِرُونَ
Wanataka kuizima nuru ya Mwenyezi Mungu kwa vinywa vyao. Na Mwenyezi Mungu atakamilisha Nuru Yake ijapokuwa makafiri watachukia.

Dini ya Mwenyezi Mungu haitegemei juu ya msaada na ulinzi wetu sisi. Ni Mwenyezi Mungu Mwenyewe ndiye ambaye atailinda dini Yake na kusaidia kazi ya Mtukufu Mtume (s). Majeshi ya Mwenyezi Mungu yanafanya kazi katika namna za muujiza kabisa. Katika tukio la pango la Thaur, kiumbe mtukufu kabisa (Mtukufu Mtume) alilindwa kwa nyumba dhaifu mno kuliko zote (utando wa buibui – Qur’ani; 29:41). Majeshi ya maadui wa Mwenyezi Mungu, pamoja na nyenzo zote ambazo wanaweza kuwa nazo, hayalingani na ya waumini ambao wanaimarishwa kwa utulivu na msaada wa majeshi yasiyoonekana.

Chanzo: Ayatullah Nasir Makarim Shirazi (chapa – Al-Amthal fi Tafsir Kitabillah)