Tafakuri ya 4, Āyat 3:37: Ukuaji Kiroho

فَتَقَبَّلَهَا رَ‌بُّهَا بِقَبُولٍ حَسَنٍ
 Basi Mola wake akamkubalia kwa kabuli nje
(Sūrat Āli Imrān, Na. 3, Āyat 37)

Wakati mama ya Maryam (a) alipokuwa anajifungua, yeye alitarajia kupata mtoto wa kiume ambaye alikuwa ameweka nadhiri ya kumtoa waqfu kwenye Baytul-Maqdis. Wakati anamzaa msichana, anamuomba Mwenyezi Mungu amkubaliye mtoto huyo. Mwenyezi Mungu anamkubalia kwa mapokezi mema yenye thamani, akionyesha heshima na huruma kwa ajili ya mama yake Maryam (a). Ni majibu kwa maombi ya kweli. Hapo kabla, kamwe mwanamke hajawahi kukubaliwa kama mtumishi wa hekalu hilo. Kwa mujibu wa baadhi ya mufasiriina, kukubaliwa huku kwa mtoto wa kike kuliwasilishwa kwa mama huyo kwa njia ya Ilhaam au uzinduo.

Mwenyezi Mungu pale anapomkubali Maryam (a) anayalea makuzi na maendeleo yake. Hili neno anbata hapa ndio neno hilohilo linalotumika kwa ukuaji wa mimea na mchakato wa kuelekea kwenye ukamilifu wa mbegu ndogo. Istilahi ya ukuaji kama hiyo imetumika katika Suratul-Fath, ambamo Mwenyezi Mungu anazungumzia kuhusu ukuaji wa wale ambao wako pamoja na Mtukufu Mtume (s): “…..kama mmea uliotoa chipukizi lake, kisha ukalitilia nguvu, ukawa mnene, ukasimama sawa kwenye shina lake…..” (Q 48:29). Uwezo wa ndani wa binadamu unaweza kulelewa kwenye ukuaji wa kimaendeleo hatua kwa hatua kuelekea kwenye ukamilifu. Ni mbegu tu ndio ambayo ina uwezo ambao unaweza kutunzwa na wakulima wa bustani wenye ujuzi na ikaweza hatimae kuwa mmea mzuri; mwanadamu anao uwezo ambao unaweza kulelewa. Chini ya uangalizi na muongozo wa viongozi watukufu wa ki-Mungu kwa hekima na elimu zao, mwanadamu anaweza akapevuka na akafanya uonekane ule uwezo ambao Mwenyezi Mungu ameuweka ndani yake.

Nabii Zakariyah (a) anawekwa katika usimamizi wa Maryam (a) kupitia upigaji kura. Wakati Maryam (a) anapokuja kwenye nyumba tukufu wazee wote wanataka kuchukua jukumu la kumlea. Hivyo Mwenyezi Mungu anaagiza mfumo ambao kupitia huo Nabii Zakariyah anachaguliwa. Hili linerejelewa kwenye aya nyingine ya Qur’ani ambamo Mwenyezi Mungu anasema: “…..Nawe hukuwa nao walipotupa kalamu zao (wakiangalia) nani katika wao atamlea Maryam…..” (Q 3:44)

Chakula alichokikuta Nabii Zakariyyah (a) chumbani kwa Maryam (a) kilileta mshangao. Hili linaweza kuthibitishwa na baadhi ya vipengele katika aya hii:

a) Ukweli kwamba neno lenyewe (rizqaan) halikuwa na mipaka ya dhahiri linaonyesha kwamba ilikuwa ni aina ya ajabu ya chakula.
b) Nabii Zakariya (a) anakiulizia chakula hicho, kuonyesha kwamba alishangazwa katika kukiona chakula hicho.
c) Maryam (a) anamjibu kwamba kinatoka kwa Mwenyezi Mungu. Vyakula vyote walivyopewa wanadamu vinatoka kwa Mwenyezi Mungu. Lakini huu sio upewaji wa kawaida wa riziki. Suala la kwamba Nabii Zakariya haulizi ni nani aliyekileta hapa kwako kunadhihirisha utambuzi wake wa mara moja tu kwamba hii ilikuwa ni neema maalum aliyopewa Maryam (a) kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Maombi yake kwa Mwenyezi Mungu yaliyofuata katika aya inayofuatia yamechipukia kutoka kwenye athari ya kuona muujiza na kumuomba Mwenyezi Mungu ambariki na yeye pia kwa neema ya kimuujiza.

Al-Amthal fi Tafsir Kitaballah inasimulia kisa cha wakati ambapo kulikuwa na njaa kali mjini Madina. Chakula kilikuwa haba na nyakati zilikuwa ngumu. Katika wakati kama huo, Bibi Fatimah (a) anakuja kwenye nyumba ya baba yake Mtukufu Mtume (s) pamoja na mkate na nyama. Mtukufu Mtume (s) anamuuliza: “Umekipata wapi hiki?” na yeye anajibu: “Kinatoka kwa Mwenyezi Mungu, Yeye anamruzuku amtakaye bila ya hesabu.” Mtukufu Mtume (s) akamshukuru Mwenyezi Mungu na akasimulia kile kisa cha Maryam (a) kwa familia yake.

Vyanzo: Āyatullāh Nāsir Makārim Shirāzī – Al-Amthāl fī Tafsīr Kitābillāh;
Aghā Muhsin Qarā’atī Kāshānī, Tafsīr-e Nūr

Tarjuma na: al-Haj Ramadhani S.K. Shemahimbo
Akademia kwa ajili ya Kujifunza Uislamu; www.academyofislam.com