Tafakuri ya 11, Āyat 39:42: Usingizi na Kifo

اَللَّهُ يَتَوَفَّى الْأَنْفُسَ حِينَ مَوْتِهَا وَالَّتِي لَمْ تَمُتْ فِي مَنَامِهَا ۖ فَيُمْسِكُ الَّتِي قَضَىٰ عَلَيْهَا الْمَوْتَ وَيُرْسِلُ الْأُخْرَىٰ إِلَىٰ أَجَلٍ مُسَمًّىۚ
إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ

Mwenyezi Mungu huzipokea roho zinapokufa. Na zile zisizokufa wakati wa kulala kwake. Huzishika zilizohukumiwa kufa, na huzirudisha nyingine mpaka ufike wakati uliowekwa. Hakika katika hayo bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanaofikiri.
(Suratuz Zumar, Na. 39, Aayaa 42)

 

Wakati wa kufa, roho hutoka kwenye mwili na huchukuliwa na Mwenyezi Mungu. Hatua hii ya roho pia inajitokeza wakati wa kulala usingizi, ijapokuwa katika namna dhaifu. Muunganisho wa roho na mwili wakati wa kulala ni mdogo sana. Inakuja kuungana tena na mwili wakati mtu anapoamka kutoka usingizini, ikirudi kwa muda uliopangwa. Fungamano la mwili na roho ni la ukweli wa udhanifu ambao sio rahisi kuuelewa. Pengine linaweza kueleweka kikamilifu mara tu pale tukiiaga dunia hii, wakati ukweli wa namna hii utakuja kuwa wazi kwetu. Qur’ani Tukufu inasema: …..basi leo tumekuondolea pazia lako, kwa hivyo kuona kwako leo ni kukali. (Q 50:22).

Kulala kumeelezwa kama ni wakati kwa ajili ya mwili kusafisha sumu unazozikusanya wakati wa kutwa nzima. Kumeelezewa vilevile kwamba ni muhimu kwa ajili ya mwili kuondoa uchovu wote na kujirudishia nguvu zake wenyewe. Hata hivyo, haya ni maelezo ya kimaumbile kwa ajili ya jambo hili la usingizi, Qur’ani katika aya hii inatupa uelewa wa kiroho wa usingizi. Ni wakati ambapo roho inauacha mwilini inaungana kwa kiasi fulani tu na mwili huo katika wakati huo.

Wakati tunapolala usingizi, ufahamu wetu unapungua na tunakuwa hatuna mamlaka tena na nafsi zetu. Utendaji wetu wa kimwili unaendelezwa lakini ufahamu wetu unahamia kwenye kiwango tofauti. Roho inawekwa katika hali tofauti yenye kubadilika: Naye ndiye anayewafisha usiku; na anakijua mlichokifanya mchana, kisha huwafufua humo ili muda umalizike….. (Q 6:60). Ule uchukuliwaji wa roho unaonyesha ukaribu na Mwenyezi Mungu, sio wa nafasi bali wa uhai. Roho inapelekwa kwenye eneo tofauti la uhai, eneo ambalo mwili haulijui. Hivyo katika usingizi wakati mwingine tunapata maono ya eneo jingine ambamo uhalisia hautegemei kwenye dunia ya kimaada.

Ayatullah Naasir Makaarim Shirazi katika Al-Amthal fi Tafsiir Kitabillah anaelezea kwamba muungano wa mwili na roho unaweza kuwa katika hatua tatu:

  1. Muungano kamili – wakati binadamu anapokuwa yuko macho. Roho inakuwa ipo pamoja na mwili na inafanya vitendo vyote pamoja nao.
  2. Muungano wa kiasi fulani – wakati mwanadamu anapokuwa amelala. Roho inauacha mwili lakini kunakuwa na mafungamano kiasi fulani nao. Kisha mtu huyo anakuwa baina ya uhai na kifo.
  3. Mtengano kamili – wakati wa kufariki. Roho inauacha mwili na kusafiri kwenda kwenye dunia nyingine. Inakuja kuungana na mwili kaburini kwa ajili ya kusailiwa na kisha inapelekwa mahali ambapo itakaa hadi Siku ya Kiyama.

Wakati Imam Zaynul-Abidiin alipofikishwa kwenye baraza la Ibn Ziyad, dhalimu huyo alimuuliza yeye alikuwa ni nani? Imam akamjibu: “Mimi ni Ali bin Husein.” Ibn Ziyad akasema: “Hivi Mwenyezi Mungu hakumuua Ali bin Husein?” Imam (a) akamjibu: “Nilikuwa na ndugu yangu ambaye pia jina lake lilikuwa ni Ali na watu wale walimuua.” Ibn Ziyad akasema: “Haikuwa hivyo, Mwenyezi Mungu ndiye aliyemuua.” Kwa kulijibu hili, Imam alisoma aya hiyo ya Qur’ani hapo juu: “Mwenyezi Mungu huzipokea roho zinapokufa, lakini Yeye siye muuaji wao.”

Mambo ya kutafakari:

  1. Mwanadamu anapitia aina dhaifu ya kifo wakati wowote anapolala usingizi. Ukumbusho ule peke yake unatutosha sisi kuwa wenye kutambua hali ya kufa kwetu na mpito wa dunia hii. Ndio hivyo kwamba tunaambiwa tusome du’a ifuatayo wakati wa kuamka kwetu kutoka usingizini: “Sifa zote ni za Mwenyezi Mungu aliyenihuisha baada ya kufa, na Kwake ndio marejeo.” Imam Muhammad al-Baqir (a) pia anasema kwamba: “Pale unapoamka kutoka usingizini sema: “Sifa zote ni za Mwenyezi Mungu aliyenirudishia roho yangu, hivyo namtukuza na kumuabudu Yeye.”
  1. Zile ndoto ambazo mtu anaziona ni tukio la roho vile inavyosafiri. Katika usingizi utambuzi wa kiwango kimoja unadhoofika na kurudi nyuma na tunaingia kwenye hali tofauti na utambuzi tofauti. Ule mpito kutoka kwenye eneo la kimaada kwenda eneo la udhanifu unahusisha upitiwaji na uhalisia tofauti wa mambo. Maono na ukumbusho wa mambo haya yanaletwa katika hali kuwa macho hivi.

Vyanzo: Ayatullah Naasir Makaarim Shiraazi (mhariri), Al-Amthal fi Tafsiir Kitabillah; Muhammadī Rayshahrī, Mizanul-Hikma.

Tarjuma na: al-Haj Ramadhani S.K. Shemahimbo